Jumatano, 18 Oktoba 2017

Tanzania na Oman wajadili vipaumbele vya ushirikiano nishati.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Mohamed Al Rumhi wamekutana  jijini Dar es Salaam na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano lengo likiwa ni kuendeleza Sekta ya Nishati nchini.

Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dar es Salaam ambapo Waziri huyo kutoka Oman aliambatana na Waziri wa Uwekezaji na Biashara ya Nje wa Oman, Naibu Waziri wa Utalii na Balozi wa Oman nchini Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania, viongozi mbalimbali walishiriki katika majadiliano hayo akiwemo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Katibu Mkuu, Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo na watendaji wengine kutoka Idara ya Nishati na Sheria.

Kwa upande wake Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dkt. Rumhi, alisema kuwa lengo la Ujumbe huo kufika wizarani ni kujadiliana na watendaji wa Wizara ya Nishati kuhusu maeneo ambayo ingependa ishirikiane na nchi hiyo ya Oman na kwamba nchi hiyo ipo tayari kushirikiana  na Tanzania.

“ Hapo zamani, Sisi Oman hatukutumia Gesi yetu vizuri kwa kuwa tulifanya haraka kuiuza nje ya nchi lakini ninyi mnayo fursa sasa ya kuitumia gesi yenu ndani ya nchi ili kutengeneza ajira pamoja na kuiendeleza kwa matumizi mbalimbali, na ikiwa ziko fursa za ushirikiano ili kuendeleza nishati hii, sisi tupo tayari,” alisema Dkt. Rumhi.

Hakuna maoni: