Jumatano, 18 Oktoba 2017

Naibu Waziri Wa Afya Aagiza Maafisa Elimu Sekondari Nchini Kuhamasisha Wanafunzi Kusoma Masomo Ya Sayansi

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Dkt,Faustine Ndugulile amewataka Maafisa Elimu Sekondari Nchini kote kuwahamasisha Wanafunzi wa Sekondari wa O-level kusoma masomo ya Sayansi ili kuwa na taifa la Madaktari na Wauuguzi wa kutosha katika Bituo vya kutolea huduma za Afya.

Naibu Waziri Dkt,Ndugulile amesema hayo wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa kusaidia na kuimarisha utoaji wa huduma za Afya ujulikanao kama "The More and better Midwives for Rural Tanzania ", unaofadhiliwa na Serikali ya Canada chini ya Shirika la JPAEGO unaotekelezwa katika Halmashauri za Mikoa minane (8) za Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi kwa kuwajengea uwezo Walimu wa Vyuo vya Uuguzi na Ukunga kuhusu uendeshaji na utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Mradi huo katika Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Bukumbi, Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza, Dkt,Ndugulile alisema ni wakati umefika sasa Watoto wajipange kusoma zaidi masomo ya Sayansi kwa lengo la kuongeza wigo mpana katika fani ya Sekta ya Afya nchini na kuboresha utoaji wa huduma ya Afya kwenye Vituo vyote vya Afya kupitia wataalamu wa Afya nq kupunguza changamoto ya Vifo vya akina mama Wajawazito na Watoto.

Alieleza kuwa changamoto ya Vifo vya Akina mama Wajawazito na Watoto ipo ambapo inakadiriwa kwamba kati ya Akinamama Wajawazito 100,000 kunatokea Vifo takribani 556 ambavyo husababishwa na baadhi yao kutojifungulia katika Vituo vya kutolea huduma za Afya na kutokuzingatia kanuni za Afya.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt,Ndugulile alibainisha matarajio na Mipango ya Serikali katika kuboresha huduma za Afya nchini ambapo inatarajia kuajiri Watumishi wapatao 3410 hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za ajira,ili kuwezesha utoaji wa huduma za Afya kuimarika katika maeneo ya Zahanati,Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya na Mikoa.

Amesema katika jitahada 
ambazo Serikali inaendelea kuchukua kwa kuboresha huduma za Afya nchini kwa kushitikiana na Wadau na Wahisani mbalimbali ni pamoja na kutoa Magari ya kubebea Wagonjwa (Ambulance) zaidi ya 50 hapa nchini na kuzigawa katika Wilaya za Mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupunguza  Changamoto y Vifo vya Wanawake Wajawazito na Watoto.

Ametoa wito kwa Wananchi wote kuthamini huduma za Afya zitolewazo na kuhudhuria katika Vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kupima Afya na kupata matibabu sahihi   na kuwataka kutotoa Rushwa kwa Watoa huduma hizo.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Juma Sweda ameshukuru Wadau kwa kutoa Mradi huo kwa wakati na kuahidi kutekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija na manufaa kwa  wananchi,na kuwataka Wauguzi na wahudumu wa Afya kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo na kanuni na maadili ya Sekta ya Afya na kutoa matokeo chanya .

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, ametoa wito kwa Wananchi wa Wilaya  hiyo kujiunga na Bima ya Afya CHF kwa kila Kaya kuchangia Tsh,10,000 na kuwezesha kupewa matibabu bure kwa mwaka mzima kwa Watu 6 kwenye familia na kueleza kuwa takwimu zinaonyesha ni Wananchi 9,100 tu ambao wamejiunga na Mfuko wa Bima ya Afya hadi  sasa na kwa upande wa utaoaji wa huduma za Afya kwa Wazee tayari Halmashauri imeshawatambua na kuwapatia Vitambulisho vya kupata matibabu zaidi ya Wazee 12,000 na zoezi linaendelea Wilaya nzima.




Hakuna maoni: