Jumanne, 17 Oktoba 2017

Marufuku uagizaji chaki nje

MKUU WA MKOA WA SINGIDA, DK. REHEMA NCHIMBI.

MKOA wa Singida umepiga marufuku taasisi za umma kuagiza chaki nje ya mkoa, badala yake umeagiza bidhaa hiyo inunuliwe moja kwa moja kutoka viwanda vilivyopo ndani ya mkoa.

Marufuku hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, Jumamosi alipokuwa akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa majengo kwenye Shule ya Sekondari ya Ilongero.

Katika ukaguzi huo ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya miaka 18 ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Dk. Nchimbi alisema Mkoa wa Singida una viwanda vya kutosha vinavyozalisha chaki.

Dk. Nchimbi alisema kutokana na wingi wa chaki zinazozalishwa mkoani humo, hakuna sababu kwa taasisi za umma kununua chaki nje ya mkoa.

“Nimeshatoa maagizo, hakuna haja ya kuagiza chaki kutoka huko Dar es Salaam chaki ambazo zinatoka kwetu, halafu zinarudi tena Singida, ni marufuku. Chaki zetu ni bora na hazina tatizo lolote, lazima mnunue hapa hapa ndani ya mkoa,” alisisitiza.

Dk. Nchimbi aliwapa ofa wateja wa nje ya mkoa watakaonunua chaki kutoka viwandani kuwa gharama ya usafirishaji ni bure kwa miezi sita, lakini baadaye utaandaliwa utaratibu wa kupunguza gharama za usafiri.

Akiunga mkono agizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Rashidi Mandoa, alisema hata baadhi ya vifaa vya ujenzi vilivyotumika katika ujenzi wa majengo ya shule yakiwamo mabati, vilinunuliwa moja kwa moja kutoka kiwandani.

Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa inayozalisha kwa wingi madini ya jipsam ambayo hutumika kutengenezea chokaa na chaki. Baadhi ya nchi jirani huchukua madini hayo kutoka wilaya za Manyoni, Itigi na Mkalama.

Hakuna maoni: