SERIKALI imeagiza kubomolewa kwa nyumba zote nchini zilizojengwa kinyume cha sheria na taratibu.
Katika kutekeleza hatua hiyo, imewaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji kuweka alama za X na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki zao za ardhi kwa dhuluma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ndiye aliyetoa agizo hilo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi.
Lukuvi aliagiza eneo lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa ulikiukwa kwa kiwango kikubwa, na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.
Hata hivyo, agizo hilo limetolewa miezi kadhaa baada ya Rais John Magufuli kusitisha bomoabomoa ya nyumba katika bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo ulitolewa kutokana na Serikali kutokuwa na taarifa za mpango wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuzibomoa nyumba hizo.
Akitangaza usitishaji huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema Rais Magufuli hakuchaguliwa kwa ajili ya kubomoa nyumba za watu na kusisitiza kuwa anataka wananchi wanaoishi maeneo halali kuachwa maana alipata taarifa kuwa huenda zoezi hilo lingekwenda zaidi mpaka kwa wananchi wasiohusika.
Waziri Lukuvi alisema tatizo la ujenzi holela linaanza pale ambapo wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji wanaacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.
“Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza wakurugenzi, maofisa ardhi, maofisa ujenzi na maofisa mipango miji kuweka X katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu maskini kwa dhuluma,” alisema Lukuvi.
Lukuvi alisema atapambana na viongozi hao pale ambapo atakuta majengo yamekithiri katika miji yao na hayana vibali vya ujenzi na baya zaidi majengo hayo yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika kiwanja cha mtu mwingine na viongozi hao wameshindwa kufuatilia kwa kuyavunja au kuyaweka alama ya X majengo hayo, kwa kuwa huu ni uzembe unaotokea nchi nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelote Stephen, alimhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atayafanyia kazi maelekezo yake kikamilifu na kwa haraka, ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
WALIOKOPA KWA MASHAMBA KULIA
Katika hatua nyingine, Lukuvi alisema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi, lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye benki ndani na nje ya nchi, lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, Dubai na kwingine duniani.
Lukuvi alisema haiwezekani mtu atumie ardhi kujipatia fedha halafu fedha hizo azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi ya Tanzania kama pori, jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.
“Kwa hiyo wizara yangu imekusudia mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka 1999, ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana,” amesema Waziri Lukuvi na kuongeza:
“Marekebisho haya tunalenga kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo katika mabenki. Kwa kuwa tathmini iliyopo inaonyesha, baada ya wawekezaji hao kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana fedha hizo hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote nchini.”
Lukuvi alisema kuanzia Novemba tatizo hilo litakwisha kabisa kwa kuwa jukumu hili zitapewa benki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika benki husika.
“Na kama benki husika haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi Serikali itamnyang’anya mkopeshwaji huyo shamba hilo kwa kuwa atakua amekiuka sheria halafu benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleza shamba lile itakuwa imekula hasara yenyewe,” alifafanua zaidi Waziri Lukuvi.
NYUMBA 58 ZABOMOLEWA
Wakati huo huo, Manispaa ya Tabora kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, imeendesha zoezi la kuwaondoa watu waliovamia eneo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora na kuvunja nyumba zaidi ya 58 za watu waliokuwa wamejenga katika eneo hilo.
Hatua hiyo ilichukuliwa jana baada ya wahusika kuombwa waondoke kwa hiari kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, lakini walikaidi kutekeleza agizo hilo na kuendelea kuishi katika la shule hiyo
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Richard Lugomela, alisema wavamilizi hao walipewa taarifa ya kuondoka katika eneo la shule muda mrefu ambao unazidi mwaka mmoja, lakini wamekuwa wakikaidi kuondoka kwa hiari.
Alisema kuwa zoezi hilo ambalo limeanzia katika shule hiyo lina lengo la kuhakikisha maeneo yote ya taasisi yaliyovamiwa yanarejeshwa na yatumike kwa ajili ya maendeleo yao ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Lugomela aliongeza hivi sasa ilikuwa ni vigumu kwa shule kama Tabora wasichana kuweka miundombinu zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa wavamizi hao.
Alisema wavamizi hao walipewa taarifa na kuomba wapewe muda wa kujiandaa ili kuondoka, lakini badala yake wameendelea kukaa kimya na kupuuzia agizo la kuwataka kuondoka katika eneo walilolivamia.
Alitoa wito kwa watu wengine wanaojijua kuwa wamevamia maeneo ya Taasisi nyingine za elimu kama Shule ya Sekondari
Milambo, Tabora Wavulana na hata yasiyokuwa yao kuanza kuondoka wao kwa hiari yao, vinginevyo watalazimika kulipia gharama za uvunjaji wa nyumba zao endapo Serikali itatekeleza zoezi la kuwaondoa.
Lugomela alisema eneo hilo lilitengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya shule ya wasichana toka mwaka 1958 na pia katika sehemu hiyo lipo eneo ambalo ni chanzo cha maji.
Mhandisi wa Maji wa Manispaa ya Tabora, Mohamed Almasi, alisema watu waliojenga katika eneo hilo hawana vibali vya ujenzi, hivyo ni wavamili ambao walipaswa kuwa wameshaondoka siku nyingi.
Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa zoezi la kuwaondoa wavamizi hao katika shule hiyo watahamia katika maeneo mengine ya taasisi na kwa watu binafsi ambao maeneo yao yamekaliwa na watu wengine kinyume cha sheria.
Almasi alitoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Tabora wanaotaka kujenga wapelekea ramani zao katika Manispaa ya Tabora ili wapatiwe kibali cha ujenzi kabla ya kuendeleza maeneo yao.
Mmoja wa waathirika wa bomoa hiyo, bomoa Hawa Katabi, alisema hakupata taarifa ya zoezi hilo jambo liliwafanya washindwe hata kuondoa mabati na matofali.
Alisema ni vema zoezi hilo linapotaka kufanyika wakapewa muda wa kutosha ili kuokoa mali zao
Kwa sasa serikali inatekeleza zoezi kubwa la ubomoaji wa nyumba zote zilizojengwa ndani ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro kuazia Kimara jijini Dar es Salaam ambapo karibu nyumba zote zilizojengwa kinyume cha sheria na taratibu kuanzia Kimara hadi Mbezi zimeshabomolewa.
Lengo la kubomoa nyumba zote ndani ya hifadhi ya barabara hiyo ambao umehusisha majengo yote yakiwamo ya binafsi na taasisi lengo lake ni kuruhusu ujenzi wa barabara ya njia sita hadi Chalinze mkoani Pwani.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni