Ijumaa, 20 Oktoba 2017

AZAM FC YATEMBELEA KITUO CHA WATOTO YATIMA CHA SEMINARI YA ILEMELA

IKIWA imesalia siku moja kabla ya kikosi cha Azam FC hakijakabiliana na Mbao, Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati muda mchache uliopita asubuhi hii wametembelea kituo cha watoto yatima cha Sekondari ya Ilemela Islamic Seminary.

Huo ni mwendelezo wa klabu hiyo katika kujenga mahusiano mazuri na jamii kwa kujali watu wenye mahitaji mbalimbali.

Zoezi hilo limehudhuriwa na msafara wote wa Azam FC uliowasili mkoani hapa Mwanza, ambapo wamepokelewa kwa heshima kubwa na viongozi wa seminari hiyo wakiongozwa na Meneja na Makamu Mwenyekiti, Sherally Hussein Sherally.

Azam FC haijaiacha mikono mitupu Seminari hiyo inayotoa elimu ya awali, msingi na sekondari kwa ngazi zote mbili, kwani imetoa msaada wa katoni 10 za Maji safi ya Uhai Drinking Water, Katoni mbili za Juice za boksi za Azam na mbili nyingine za kopo pamoja na pakiti mbili za pipi.

Uongozi wa seminari umeipongeza na kuishukuru timu hiyo na Kampuni kwa ujumla ya Azam kwa moyo wa huruma waliouonyesha na kuamua na kuitakia mafanikio mema kwenye mechi wanazocheza.



Hakuna maoni: