Jumatatu, 16 Oktoba 2017

Amnesty na HRW wasema polisi waliwaua watu 33 Nairobi wakati wa uchaguzi

Polisi nchini Kenya waliwaua watu 33 katika mji mkuu wa Nairobi wakati wa ghasia na maandamano ya upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti, mashirika mawili ya haki za kibinadamu yamesema.

Kwenye ripoti mpya Amnesty International na Human Rights Watch (HRW) wamesema polisi walihusika moja kwa kwa moja katika mauaji hayo.

Kuna taarifa nyingine ambazo hazijathibitishwa zinazodokeza kwamba huenda watu wengine 17 waliuawa jijini Nairobi wakati wa ghasia hizo.

Mashirika hayo mawili, ambayo yanasema kwa jumla watu 67 wameuawa na polisi kote nchini Kenya kipindi hicho, yamewatuhumu polisi kwa kuongeza uhasama kwa kutumia nguvu kiasi katika maeneo ambayo ni ngome za upinzani ambayo yalitarajiwa kukumbwa na maandamano.

Aidha, yanasema kutumia nguvu kupita kiasi limekuwa jambo la kawaida kwa polisi nchini Kenya.
"Wachunguzi wetu waligundua kwamba polisi wenye silaha - wengi kutoka Polisi wa Kupambana na Fujo (GSU) na Polisi wa Utawala (AP) - walifanya operesheni maeneo ya Mathare, Kibera, Babadogo, Dandora, Korogocho, Kariobangi, na Kawangware jijini Nairobi kati ya Agosti 9 na 13," taarifa ya mashirika hayo inasema.

"Waliwafyatulia risasi baadhi ya waandamanaji moja kwa moja na wakati mwingine walifyatua risasi kiholela kuelekea kwenye umani.

"Waathiriwa na walioshuhudia waliwaambia wachunguzi wetu kwamba waandamanaji walipokuwa wanakimbia kutoroka, polisi waliwaandamana, wakavunja milango kwa nguvu na kuwakimbiza baadhi ya waandamanaji vichochoroni, wakawapiga risasi na kuwapiga wengine vibaya hadi wakafa."

Mashirika hayo yanasema polisi walionyesha ukatili pia kwa wanahabari na watu wa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu waliojaribu kupiga picha na video za matukio hayo, wakati mwingine wakiharibu kamera zao.

Naibu inspekta mkuu wa polisi George Kinoti hata hivyo amekanusha tuhuma hizo zilizotolewa na mashirika hayo akisema ni "za kupotosha na zimetokana na taarifa za uongo."
Muungano wa upinzani umekuwa ukifanya maandamano mara kwa mara kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi.

Ijumaa wiki iliyopita, watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi mjini Bondo magharibi mwa Kenya baada ya kudaiwa kujaribu kuvamia kituo cha polisi wakati wa maandamano ya Nasa.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.

Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.

Tume ya uchaguzi ilitangaza tarehe mpya ya uchaguzi kuwa 26 Oktoba lakini Bw Odinga alijiondoa wiki iliyopita akisema mageuzi ambayo yalifaa kutekelezwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki hayajatekelezwa.




Hakuna maoni: