MFANYABIASHARA HERBINDER SETHI.
MFANYABIASHARA Herbinder Sethi amewasilisha maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu Tanzania, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi dhidi ya kesi ya kutakatisha fedha inayomkabili kwa madai anasumbuliwa na maradhi yanayohitaji kuwa chini ya uangalizi wa madaktari wataalamu.
Kadhalika, amedai kutokana na kufanyiwa upasuaji mara mbili na kuwekewa puto tumboni, anahitaji kuwa chini ya uangalizi wa madaktari wake na huduma hiyo itampa nafasi ya kuhudhuria kesi hiyo inayomkabili akiwa timamu.
Maombi hayo yalisikilizwa jana mbele ya Jaji Winfrida Koroso.
Katika hoja zake zilizowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wake, Joseph Makandege, anaomba mahakama impe dhamana kwa sababu ni mgonjwa.
Maombi hayo namba 29/2017, yaliwasilishwa chini ya hati ya kiapo kwamba sababu za kuomba dhamana hiyo ni mgonjwa, anahitaji kuwa karibu na wataalamu wa afya. Vinginevyo kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha.
Alidai pamoja na wakili wake kumshauri kesi ya kutakatisha fedha haina dhamana, lakini mahakama inaweza kuchepuka na kumpa dhamana hiyo kwa sababu ana wadhamini wa kuaminika.
Alidai alifanyiwa upasuaji mwaka 2016 na mwaka huu mara mbili tofauti Afrika ya Kusini na kuwekewa puto tumboni ambalo linatakiwa kuangaliwa na daktari mtaalamu mara kwa mara.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Dk. Zainabu Mango, uliwasilisha pingamizi la awali kwamba hati ya kiapo ya mshtakiwa ina mapungufu ya kisheria.
Dk. Mango aliomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo dhidi ya mshtakiwa kutokana na mapungufu ya hati ya kiapo.
Jaji Koroso alisema mahakama yake itatoa uamuzi Septemba 26, mwaka huu.
Sethi na mshtakiwa mwenzake, James Rugemalira, wanakabiliwa na tuhuma za kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Seth na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha serikali hasara ya dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni