Jumapili, 24 Septemba 2017

Kocha Julio asema tukutane Ligi Kuu msimu ujao

Ushindi wa pili mfululizo ilioupata Dodoma FC ugenini dhidi ya wenyeji Biashara United mkoani Mara, imezidi kumpa jeuri kocha Jamhuri Kiwhelo maarufu kwa jina la Julio ambaye ametamba kushinda mechi zote za raundi ya kwanza za Ligi Daraja la Kwanza.

Dodoma FC ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 wakiwa ugenini kwa bao la kipindi cha pili la kiungo wake Rajabu Mgalula na kufikisha pointi 6 huku mchezo ujao wakitarajiwa kusafiri hadi mkoani Mwanza kucheza na Alliance Oktoba Uwanja wa CCM Kirumba.

Julio alisema kila mchezo ni fainali na kuwa licha ya kupata ushindi katika mazingira magumu dhidi ya Biashara United waliocheza uwanja wao wa Karume kilichowasaidia kuibuka na ushindi huo ni dhamira walioyojiwekea kwa kila mchezo ni lazima kupata ushindi.

Kocha huyo asiyeishiwa maneno mbali na kutangaza hatari kwa timu pinzani lakini pia alisisitiza endapo mechi zote zitachezeshwa kwa haki na timu kushinda kwa uwezo binafsi. haoni timu ya kuizuia timu yake kushinda mechi zote 7 za raundi ya kwanza.

Hakuna maoni: