Jumatano, 20 Septemba 2017

Afariki bwawani akiogelea

KIJANA mmoja mkazi wa Kijiji cha Mtindiro Kata ya Mtindiro wilayani Muheza mkoani Tanga,  Yasin Hussen (22) amefariki dunia kwa kuzama katika bwawa la  kuhifadhia maji lililopo Buhuri wakati akiogelea.

Tukio hilo lilitokea  juzi jioni eneo la Buhuri Kata ya Mtindiro.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema Yasin alikwenda katika bwawa hilo la kuhifadhi maji kwa lengo la kuogelea akiwa peke yake.

Wakulyamba alisema wakati akiogelea, alizidiwa na maji hayo kisha kuzama, hivyo kupoteza maisha.

Hata hivyo, alisema marehemu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifafa na kwamba katika tukio hilo alizama baada ya kushikwa ghafla na ugonjwa huo.

Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa hiyo za marehemu kuzama walianza  msako wa kumtafuta katika bwawa hilo na
kufanikiwa kumpata majira ya mchana.

Mkuu wa upelelezi wa jeshi la polisi wilaya ya Muheza, Jonas Sira, alifika katika sehemu ya tukio hilo huku akiwaonya vijana na watoto wanaoishi karibu na bwawa hilo wasiogelee kwa kuwa ni rahisi kuzama na kupoteza maisha.

Hakuna maoni: