Jumatano, 10 Januari 2018

Mwendokasi wazungumzia athari zinazoukumba Mradi huo


SIKU moja baada ya kunyesha mvua kubwa jijini Dar es Salaam na kusababisha mafuriko, waendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka, maarufu Mwendokasi, wameeleza athari hasi ambazo zimekuwa zikiukumba mradi huo kunaponyesha mvua kubwa.


Juzi, kampuni ya mabasi hayo (UDA-RT) kupitia mkuu wake wa kitengo cha mawasiliano, Deus Bugaywa, ilitangaza kusitisha kwa muda huduma zake za mabasi kutokana na kujaa maji juu ya daraja la Mto Msimbazi kwenye barabara ya Morogoro.

Nipashe ilimtafuta Bugaywa jana kuzungumzia kwa undani athari ambazo zinazoukumba mradi huo, hususani kutokana na kujengwa kwa kituo cha mabasi yake kwenye eneo la maji ambalo ni njia kuu ya maji ya Mto Msimbazi na pia ni mkondo wa upumuaji wa bahari.

Katika mazungumzo hayo, Bugaywa alikiri kituo cha mabasi hayo hakiko eneo salama na limekuwa likiwasababishia hasara kubwa kipindi cha mvua kubwa zinazosababisha kufurika maji kwenye eneo la Jangwani jijini.

"Athari ni nyingi, kwa mfano jana (juzi) tulisitisha huduma kwa takriban saa mbili kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa tano. Kihesabu, hiyo ni hasara maana tumepoteza mapato," Bugaywa alisema na kuongeza:

"Pia inaongeza gharama za uendeshaji. Kwa mfano jana (juzi) magari yalikuwa yamekwama ikabidi watu watolewe kwenye mabasi na huduma zikasitishwa. Huduma kwa magari yetu nazo zikakwama, magari ambayo yaliharibika kutokana na maji ya Jangwani hayakufanyiwa 'service'."

Alisema mafuriko pia yamekuwa yakisababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme kwenye kituo na kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za mradi hasa matengenezo ya magari.

"Kumbuka hata gereji yetu pale inahitaji umeme kwa kiasi kikubwa maana vifaa vingi ni vya umeme. Athari nyingine ni usumbufu kwa abiria unaosababisha kampuni kupoteza kuaminika. Sisi kama watoa huduma, tunategemewa na watu na tunapaswa kujali muda wao,” alisema.

Aliongeza kuwa: "Ukisitisha huduma hiyo, maana yake unakwamisha shughuli za wananchi. Kila safari ya mtu ina sababu yake. 'Credibility' (uaminifu) inashuka kwa sababu lengo la mabasi haya ni kusafirisha na kuhudumia watu, sasa inapotokea huduma zinasitishwa ni changamoto kubwa sana.

"Kwa sababu masika yataendelea kuwapo na hali ndiyo hiyo Jangwani, tunafikiri miundombinu iangaliwe. Tunafahamu serikali inafanyia kazi Bonde la Mto Msimbazi, lakini hili siwezi kulisemea sana kwa sababu liko chini ya mamlaka nyingine, lipo kwa serikali.

Pia alisema wamekuwa wakilazimika kulipa fedha ya ziada kwa mafundi wa mabasi ili wafanye kazi hadi usiku kuyafanyia matengenezo mabasi pale mvua kubwa na kukiathiri kituo.

Alishauri mamlaka zinazohusika na miundombinu ya mradi huo ziangalie namna ya kuboresha mazingira ya kituo au kupata eneo jingine kwa ajili ya kituo cha mabasi hayo.

Katika mazungumzo hayo, Bugaywa hakuwa tayari kuweka wazi mapato yaliyopotea juzi na kutokana na kusitishwa kwa muda kwa huduma za mabasi hayo.

Hata hivyo, Mei 30, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliliambia Bunge kuwa mradi wa mabasi hayo umekuwa na mafanikio makubwa na kubainisha kuwa idadi ya watu wanaotumia huduma hiyo imepanda kutoka 76,000 kwa siku Mei 2016 hadi 180,909 kwa siku Machi 2016.

Kwa mantiki hiyo, kila siku mabasi hayo huingiza Sh. milioni 117.59 ikiwa watu wote watalipa nauli ya Sh. 650 kila mmoja (bila kujali wanafunzi na safari za Kimara-Mbezi) ambazo nauli zake ni Sh. 400.

Kwa kuzingatia takwimu hizo za Dk. Mpango, kwa saa mbili ambazo huduma za mabasi hayo zilisitishwa jana, waendeshaji wa mradi huo walipoteza Sh. milioni 12.4 kwa kuzingatia kwamba mabasi hayo hufanya kazi kwa saa 19 kwa siku kuanzia saa 11 alfajiri hadi saa sita usiku.

Kwa mujibu wa Bugaywa, mradi huo kwa sasa una mabasi 140.

Hakuna maoni: