Alhamisi, 11 Januari 2018

Mapya yaibuka uchaguzi Mkuu wa Kenya

Mkuu wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi mkuu wa Agosti na Oktoba 2017 amesema mipango yake kuja nchini kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kuhusu uchaguzi huo iliwekewa vizingiti.

Mwangalizi huyo, Marietje Schaake, akizungumza kupitia televisheni Jumatano asubuhi kutoka Brussels, Ubelgiji alisema amelazimika kusoma ripoti yake kutokea Bunge la Umoja wa Ulaya ili kutimiza mwongozo wa kuwasilisha ripoti miezi mitatu baada ya uchaguzi.

“Tukio hili ni moja ya nyakati chache sana kwamba ripoti ya mwisho ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya inasomwa kwenye Bunge la Ulaya badala ya nchi husika ambako ulifanyika uchaguzi — Kenya,” alisema Schaake.

“Tulijiandaa kikamilifu kusafiri hadi Nairobi wiki hii kuwasilisha ripoti ya mwisho ikiwa na mapendekezo yetu kwa serikali ya Kenya pamoja na wadau wengine, bila shaka muhimu zaidi ni wananchi wa Kenya Kenya.”

Makubaliano

“Tumebaini, hata hivyo kwamba serikali ya Kenya haikuwa tayari kutupokea kwa kuzingatia makubaliano tuliyotiliana saini kati ya Umoja wa Ulaya na Kenya; kwa sababu hayo ndiyo yanabainisha kwamba tutawasilisha ripoti yetu ya mwisho katika kipindi cha miezi mitatu tangu Siku ya Uchaguzi,” alisema mwanasiasa huyo kutoka Uholanzi.

Baada ya maelezo hayo mwanamama huyo alianza kusoma walichoshuhudia wakati wa uchaguzi na muhtasari wa timu wenye mapendekezo 29

Miongoni mwa mambo yaliyopewa uzito ni watu kulipwa fedha ili wahudhurie mikutano ya siasa, matumizi ya raslimali za serikali kufanikisha kampeni, wanasiasa kuzitisha taasisi muhimu huru na kukosekana mfululizo kuaminika kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Vilevile, aligusia vurugu zilizosababishwa na polisi na raia wakati wa kipindi cha uchaguzi huo na akadokeza “Wakenya hawakufurahia kikamilifu haki yao kidemokrasia”.

Kwa maoni yake, hatua ya Wakenya kuamua kulinda amani ndiyo imeiepusha nchi kutumbukia kwenye machafuko.

“Ukweli kwamba Kenya haijatumbukia kwenye hali mbaya imechangiwa na Wakenya wenyewe,” alisema.

Hakuna maoni: