Upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, inayomkabili mfanyabiashara, Ndama Shabani Hussein maarufu kama Pedeshee Ndama mtoto ya Ng'ombe, umeieleza Mahakama kuwa wanasubiri nyaraka kutoka nchini Australia.
Ndama anakabiliwa na mashtaka matano katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha dola za kimarekani 540,000.
Wakili wa Serikali, Estazia Wilson leo Jumatano ameeleza mbele ya hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa kuwa wameshapeleka maombi kwa ajili ya kupata nyaraka hizo.
"Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa yupo mbele ya mahakama yako kwa ajili ya kuendelea na kesi, lakini upande wa mashtaka tunasubiri nyaraka kutoka Australia ambazo tuliziomba, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili kutajwa," amesema.
Baada ya maelezo hayo, upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Jeremia Mntobesya aliomba upande wa mashtaka uharakishe upelelezi katika kesi hiyo.
Hakimu Nongwa alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, mwaka huu itakapotajwa na kwamba mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni