Jumatano, 10 Januari 2018

CCM yatamba kuibuka na ushindi Longido


Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, kimetamba kuibuka na ushindi wa asilimia 96 katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Longido kutokana na kuimarisha kampeni zake, baada ya kuongeza nguvu ya makada wake, Christopher Ole Sendeka na Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma.

Akizungumza na mwanandishi wa habari hii jana, kabla ya mkutano wa kampeni katika mji wa Namanga, katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoani hapa, Shaaban Mdoe alisema watashinda kwa asilimia 96 katika uchaguzi huo.

“Baada ya Chadema kuweka mpira kwapani, tutashinda kwa asilimia 96 na sasa tunachofanya ni kutembea jimbo zima kusikiliza kero za wananchi ambazo tutazipeleka ndani ya vikao vya chama na serikalini ili zipatiwe ufumbuzi,” alisema.

Mdoe alisema katika mikutano ya kampeni, pia mgombea wa ubunge wa chama hicho, Stephen Kiluswa anatakiwa kutumia fursa hiyo kupokea kero zote na kuzifikisha bungeni ili kutatua kero za wananchi.

“Kimsingi tunaendelea vizuri, tupo na timu nzuri ya kampeni. Tupo na Christopher Ole Sendeka, Msukuma, mwenyekiti wa (CCM) Mkoa Arusha, Loota Sanare na baadhi ya wenyeviti wa CCM wa wilaya za mkoa wa Arusha,” alisema. Katika uchaguzi huo ambao utafanyika Jumapili wapigakura 57,808 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 175.

Akizungumza na mwandishi wa habari, msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Juma Mhina alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika.

Alisema katika uchaguzi huo kutakuwa na wasimamizi 700 na polisi 175 ili kuimarisha ulinzi.

Mkurugenzi wa haki za binadamu wa CUF wilayani Arusha, Abdalah Shabani alisema chama hicho kimejipanga kushinda na kujiimarisha kupitia kampeni hizo. “Kampeni zetu zinakwenda vizuri, alikuja Profesa Lipumba (Ibrahim) amefanya kampeni nzuri na baadhi ya wabunge na kilichotufurahisha ni watu wengi wanajiunga CUF,” alisema. Katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili vyama vitakavyochuana ni CCM, TLP, TADEA, Demokrasia Makini, AFP, CCK, NRA, Sauti ya Umma na CUF upande wa Profesa Lipumba.

Hakuna maoni: