Jumamosi, 16 Desemba 2017

Wataalam wa Afya wasema lipo tishio kubwa watoto kupata maradhi ya Moyo, Pumu


 Wataalamu wa afya wamesema lipo tishio kubwa la watoto kupata magonjwa yasiyoambukizwa hasa moyo na pumu.

Takwimu zilizokusanywa na Taasisi ya Kiraia ya Kinga dhidi ya magonjwa (CCP Madicine Medical Centre) zinaonyesha kati ya watoto 100 waliopimwa katika manispaa ya Ilala, 20 wanasumbuliwa na pumu wakati 10 wana magonjwa ya moyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa mchakamchaka kwa wanafunzi shuleni, mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukizwa mkoa wa Dar es Salaam, Dk Digna Riwa alisema aina ya maisha ya watoto siku hizi ndiyo inayowaweka kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo.

Alisema watoto wengi wanakosa muda wa kufanya mazoezi huku wakipatiwa vyakula vya mafuta, jambo linaloendelea kuhatarisha maisha yao.

Awali, mkurugenzi wa manispaa ya Ilala, Nito Pallera alisema atasimamia kuhakikisha wanafunzi wa manispaa hiyo wanatengewa muda wa mchakamchaka kama njia ya kupambana na magonjwa hayo.

Alisema njia pekee itakayowawezesha kutimiza malengo yao ni afya njema inayotokana na ufanyaji wa mazoezi, lishe bora na elimu nzuri.

Mkurugenzi wa Taasisi ya CCP, Dk Frank Manase alisema mwaka jana walifanya zoezi la kupima afya za watoto shuleni na kupata matokeo yaliyowashtua, hivyo wakaanzisha kampeni ya mchakamchaka kama njia mojawapo ya kuwasaidia watoto hao.

Hakuna maoni: