Charles James
God Zillah ni kweli umezikubali Stress za Bill Nas?
MWAKA 2010 ndio mwaka ambao baada ya kitambo kirefu cha akina Diplomatic, Kwanza Unit na wakali kibao nilishuhudia urejeo na muamko mkubwa wa Hip Hop jijini Dar es Salaam. Tutarudi hapa baadaye.
Unapozungumzia wasanii wa kwanza wa Hip Hop kutamba nchini na haswa Dar, basi wajina ya wakali kutoka makundi ya Diplomatic iliyokuwa inaundwa na watu kama Saigoni na Kwanza Unit iliyokuwa na watu kama Chief Ramso, D-Rob na KBC yatatajwa.
Baada ya hapo ni kama Dar es Salaam ilipoteza nguvu ya Hip Hop nchini huku ikionekana kuzalisha wasanii wengi wanaofanya muziki wa kuimba, Bongo fleva na R&B.
Majina kama TID, Q Chillah na Dully Sykes yalikuja kufanya mapinduzi ya muziki na kuteka mashabiki kutokana na staili zao walizoingia nazo kwenye game.
Licha ya Hardcore Unit na X PLastarz kutamba Arusha lakini ni miaka ya 2000 kuja huku tulipo ndipo Jiji hilo lilipogeuka kuwa la Hip Hop huku wasanii wake wakitengeneza nguvu yao na kulitambulisha jiji lao kwenye ramani ya muziki.
Joh Makin aliongoza kikosi chake cha River Camp
sambamba na Nikki wa Pili, Bonta Maarifa, Shaa Bang na Rama Dee, Lord Eyez akitamba na Nako 2 Nako akiwa na wanae, Bou Nako, G Nako na Ibrah Hustlers.
Ukipandisha Kijenge Juu, JCB na Chindo Man walikuwa wakipambana kuiweka Watengwa katika ramani ya muziki ingawa hawakuweza kufanikiwa kama wenzao wawili hapo juu.
Usisahau pia kuhusu Mapacha K na D kutoka Maujanja Saplayaz na Stopa Ryhmez yule mbabe wa ‘Tantwista’ aliyetamba na ngoma ya Staili Tatu wote waliyoka A Town.
Mwanza pia ilionekana kuwa ni Jiji la Hip Hop kulinganisha na Dar kutokana na nguvu aliyokuwa nayo Fid Q, Kala Jeremiah . Achana na huyu Lil K ambaye wengi wanamfahamu kama Young Killer Msodoki kuibuka.
ZILLAH NA LUNDUNO WANAIRUDISHA DAR MCHEZONI
Nilikuahidi kurejea baadae kukueleza namna ambavyo kuliibuka kundi la wasanii wa Hip Hop, 2010 na kurudisha nguvu ya muziki huo jijini Dar es Salaam kama ambavyo walifanya Diplomatic, Kwanza Unit na Hasheem Dogo.
God Zillah sambamba na Familia ya Lundono iliyoundwa na Nikki Mbishi, Stereo Singasinga na One Incredible waliibuka kwa nguvu kubwa huku wakifanikiwa kuteka mashabiki wengi wa Rap kutokana na uwezo waliokuwa nao kwenye michano na uandishi.
Sasa watu wakawa wanafanya ulinganisho wa ‘madogo’ waliokuwa wametoka Lundono, Zillah dhidi ya watoto wa Arusha, Joh Makin na wanae wa Weusi.
Zillah alifanikiwa kutoka kimuziki kulinganisha na wenzake na hiyo ni kutokana na uwezo wake wa kutoa ‘hit song’ ambazo zilikuwa zikiendana na soko la muziki lakini pia uwezo wa kufanya mitindo huru ‘Free Style’ ukizidi kumpaisha.
Alifanikiwa kutengeneza ngoma nyingi akautambulisha muziki wake na kuiweka Empire yake ya Salasala juu kiasi kwamba hata wale ambao walikuwa hawapajui sasa walianza kutambua kuna kona Dar inaitwa Salasala na kuna msanii anatokea huko anaitwa God Zillah.
Kutoka 2010 Zillah alifanikiwa kutengeneza jina lake kutoka kuwa msanii wa mdogo na kuwa Staa mkubwa wa Rap huku wengi wakimuona kama 50 Cent wa Bongo.
Alifanana na wakali wa Marekani kwa namna ambavyo alijiweka kuanzia uwezo wake wa kuchana ‘Free style’, matumizi mengi ya kiingereza pale alipozungumza na kwenye ngoma zake.
Kukutana na Prodyuza, Marco Chalii wa Studio za MJ, kukazidi kumpa kiki mjini na zaidi walikutana kipindi ambacho Chalii anatamba na tuzo zake kama Mtayrishaji bora wa Muziki Bongo.
Kwanini asitambe, Rapa gani angetaka kukutana na Zillah kwenye Interview alafu akapona kwenye Free Style, Zizi kama mwenyewe anavyojiita alikuwa kwenye ubora wake na kilele cha mafanikio yake kwenye game.
Kama alishindwa kuwekeza kama alifanikiwa, kama hakuweka akiba, yote anajua yeye lakini kwa muda ambao sauti yake ilisumbua masikio yetu basi anapaswa kuwa mbali kwa sasa kimaisha.
Zillah hakuwahi kukosa zile Shoo kubwa za mara moja kwa mwaka, alitembea karibia kila mkoa na zile shoo, alipata ‘airtime’ nyingi za Radio na TV.
Kama alichezea kama aliwekeza anafahamu mwenyewe.
ZILLNAS INA UKWELI WOWOTE?
Kwa miaka miwili sasa, Zillah hasikiki, Zillah haonekani, Zillah amepwaya na hata akitoa ngoma siyo Zillah yule wa La Kuchumpa na Joti wake.
Zillah yule aliyesumbua Radio zote kwa Free Style na ukali wa mitindo, Zillah aliyeiweka Salasala kwenye ramani sasa haonekani, amepoa na ni dhahiri anasumbuliwa na jambo kichwani mwake.
Miezi kadhaa nyuma nilibahatika kusikiliza You heard ya Soudy Brown kwenye XXL ya Clouds Fm ambapo Zillah alikuwa akihojiwa kuhusiana na bifu lake na Mkali mwingine wa Hip Hop, Wakazi.
Namna ambavyo Zillah alikuwa akijibu maswali namna ambavyo alizungumza nilihisi hatari katika maisha yake ya kisanii.
Nilishtuka na sikutarajia kusikia Zillah akizungumza kama mtu ambaye haeleweki, anajichekesha hovyo huku akizungumza vitu ambavyo Soudy hakumuuliza.
Nikaweka nukta nikiamini pengine kutokana na ‘nature’ ya kipindi kukaa kiubuyu ubuyu labda ndio sababu ya Zillah kuzungumza vile.
Siku chache mbele nikafanikiwa kuiona Interview yake yeye na Wakazi ambaye wana bifu katika kituo cha Times Fm.
Zillah yule yule niliemsikia kwa Soudy ndio niliyemuona na kumsikia Times, Zillah ambaye kisaikolojia anaonekana kuathirika, na hii niliipima kutokana na namna alivyokuwa akizungumza na kujibu maswali.
Wakati Wakazi yeye alionekana kutulia, Zillah alikuwa akiongea hovyo, akitoa maelezo ambayo hakuulizwa maswali yake, na zaidi hata walipoekewa mdundo sikumuona yule Zillah ambaye alikuwa akizibaka beats.
Chanzo kikubwa cha ugomvi wake na Wakazi kinatajwa kuwa ni diss ambayo Wakazi aliitoa kwa Zillah kuwa ameathiriwa na ujio wa Bill Nas ambao umekuja kutikisa nafasi yake.
Siyo jambo la kumung’u nya maneno kuwa Bill Nas amekuja kuiteka nafasi ya Zillah, huo ni ukweli ambao upo.
Staili ya muziki ya Bill, voko na hata sauti ni wazi vinafanana na Zillah, alichokiongezea yeye ni kuifanya kwa usasa zaidi huku akijua kucheza na Soko la muziki linataka nini.
Kwa hiyo kama kweli Zillah ana stress juu ya Bill ni jambo la kuchekesha kwa sababu kama msanii mkubwa ambaye ana uzoefu wa game angeweza kubadilika na kuangalia namna ambavyo anaweza kutoka kwa namna nyingine na kulibakisha jina lake kwenye ‘fame’.
Sasa namna ambavyo anazidi kujiweka ndivyo anavyozidi kupotea, kuingia kwenye bifu zisizo na maana kutamtafuna mwenyewe bila kufahamu.
Zillah unapaswa kuamka na kutambua thamani na kipaji chako bado vinahitajika kwenye game, tuliza akili na uangalie namna ambavyo unaweza kulirudisha jina lako pale lilipokuwa.
Igy Azalea aliibuka na watu kumfananisha na Nick Minaji lakini ameshindwa kumshusha Nick, August Alsina alipotoka wengi tulimuona kama mtu anaekuja kuuteka muziki wa Chris Brown lakini imeshindikana.
Rihanna alitajwa kama msanii anaekuja kumnyima usingizi Beyonce lakini leo hii bado anaisoma namba kwa Queen Bee, Zillah amka na uoneshe hua msongo wa mawazo na ZillNas.
Namna unavyojiweka mbele ya mashabiki haswa unavyojibu maswali kwenye Interview zako ndivyo unazidi kujichimbia kaburi. Amka na uoneshe ule ubora wako ulioirudisha Dar kwenye ramani ya Rap ukiwa na washikaji zako wa Lunduno.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni