Jumanne, 28 Novemba 2017

Waziri mkuu atoa onyo kali

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali haitawavumilia watu wote wanaotumia vibaya fedha za umma ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi zikiwemo fedha za mfuko wa Ukimwi.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo wakati akifungua kongamano la kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika jijini Dar es Salaam. Mh. Majaliwa amesema serikali itawashughulikia wote wakiwemo wale wanaotumia vibaya fedha za Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi.

“Nitoe wito kwa Bodi ya Mfuko huu na watendaji wake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha hizi ili ziweze kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko huu”, amesema Waziri Mkuu.

Ameongeza kuwa mfuko huo unalenga kufanikisha ukusanyaji wa fedha za kutosha ambazo ni muhimu wakati huu ambao taifa linaazimia kumaliza ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Waziri Mkuu amesisitiza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhamasisha wananchi, wadau na sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu.

Hakuna maoni: