Jumatano, 29 Novemba 2017

Wavuvi wapunguziwa tozo na Ushuru Mafia


Halmashauri ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani imepunguza ushuru na tozo mbalimbali kwa wavuvi, wafanyabiashara na watumiaji wengine wa mazao ya bahari.

Hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega kuiagiza halmashauri hiyo kuondoa malalamiko ya ushuru ili kuwaongezea unafuu wa maisha wananchi wa chini.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Erick Mapunda alisema wilaya hiyo imefanikiwa baada ya kufanyika kikao cha baraza la madiwani kilichoridhia kupunguzwa kwa tozo na ushuru huo.

“Tulipewa siku saba kuhakikisha mtambo wa barafu unafanya kazi, na ndani ya siku tatu umewaka na unafanya kazi. Bei ya barafu ni ndogo, pia bei ya kuhifadhi samaki imepungua kutoka Sh500 hadi Sh100 kwa siku,” alisema.

Mapunda alisema mabadiliko ya tozo na ushuru yaliyofanyika yamepunguza mapato ya halmashauri hiyo kutoka Sh707.6 milioni hadi Sh383.06 milioni.

“Hii inatokana na kupunguza kwa tozo za mazao ya bahari pamoja na mabadiliko ya bei elekezi. Ili kufidia upungufu huu mkakati uliopendekezwa ni kuongeza usimamizi na kubuni vyanzo vingine,” alisema.

Akielezea ushuru na tozo hizo, Mapunda alisema kamba kochi bei imepungua kutoka Sh2,250 kwa kilo moja hadi 1,500, kaa hai Sh2,250 hadi Sh1,050, dagaa Sh80 hadi 50, Vumbi dagaa Sh80 hadi Sh25, ngisi Sh200 hadi Sh135 na samaki wabichi Sh100 hadi Sh50.

Hata hivyo, alisema wavuvi waliokuwa wanauza samaki kwa hasara wakihofia kuoza kwa kukosa fedha za kuhifadhia kwenye mitambo ya watu binafsi wataweza kufanya hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Annunduma alisema kupungua kwa bei hiyo kutawarejesha wafanyabiashara na wavuvi waliokuwa wamekimbilia maeneo mengine.

“Ushuru na tozo vimepungua, nia yangu tutaungana kuijenga wilaya yetu kwa kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii,” alisema.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mohamed Gomvu aliwataka wavuvi na watumiaji wengine wa rasilimali za bahari kutunza mazingira ili shughuli wanazozifanya ziwe endelevu.

“Hakutakuwa na maana kama tutaondoa ushuru na tozo halafu nyie mnaharibu mazingira, mwisho wa yote umaskini utaendelea kututafuna. Lazima tuyatunze mazingira yetu ya bahari,” alisema.

Awali, wafanyabishara na watumiaji wa rasilimali za bahari waliiomba wilaya hiyo kupunguza tozo na ushuru mbalimbali ili kuwawezesha kumudu gharama za maisha ambazo zipo juu.

Hakuna maoni: