Jumamosi, 4 Novemba 2017

Wafuasi 12 wa Chadema washikiliwa na jeshi la Polisi

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia wafuasi 12 Chadema  mkoani Arusha kwa kosa la kumshambulia mgombea udiwani  wa CCM   Kata ya Muriet, Francis Mbise.

Miongoni mwa watu waliokamatwa ni pamoja na Kaimu Katibu wa chama hicho  wilayani hapa, Innocent Kisanyage

Mbali na kushikiliwa Kwa wafuasi hao pia jeshi hilo linashikilia  gari la matangazo la chama hicho ambalo limekuwa likitumika kutangaza mikutano ya Chadema katika kampeni za uchaguzi mdogo jijini hapa.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha, (RPC) Charles Mkumbo amethibitisha kushikiliwa kwa wafuasi hao na kusema kwamba walikamatwa jana usiku  katika eneo la FFU kwa Morombo.

Mkumbo, amesema kwamba wafuasi hao waliwavamia wafuasi wa ccm  wakati wakitoka katika mikutano ya kampeni eneo la Muriet na kuanza kuwashambulia .

Amesema kwamba katika vurugu hizo wafuasi hao wamemshambulia Mbise na kumuumiza sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo amekimbizwa hospitalini kupatiwa matibabu.

Amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Edwin Christopher, Yohana Mtaa, Paschael Lucas, Nasoro Ally, Godson Samwel, Joram Baraka, Bayo Shana, Cecilia Lucas, Aurelia Lucas ,Rehema Juma, Amina Musa sanjari na Kisanyage.

Mkumbo, amesema kwamba jeshi lake bado linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili.

Hakuna maoni: