Jumanne, 7 Novemba 2017

Vikao vya Bunge kuendelea kesho

Dodoma. Vikao vya Bunge vya Mkutano wa tisa vinaanza kesho  mjini Dodoma ambapo miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2018/19.

Akizungumza leo Novemba 6,Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai amesema kuwa bunge litakaa kama kamati ya mipango kukidhi ibara 63 (3C) ya Katiba kujadili na kuishauri Serikali kuhusu mpango huo.

 “Shughuli nyingine zitakazofanyika katika mkutano huu ni kutakuwa na kiapo cha uaminifu kwa Janeth Masaburi ambaye ameteuliwa na Rais kuwa mbunge,” amesema.

Amesema pia kutakuwa na maswali 125 ya kawaida na wastani wa maswali 16 papo kwa papo kwa waziri mkuu.

Pia amesema kutakuwa na miswada ya serikali minne ambayo itajadiliwa na Bunge na kusomwa katika hatua zote.

Ameitaja  miswada hiyo kuwa ni Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano la Tanzania wa mwaka 2017, Muswada wa Sheria wa Wakala wa Meli wa mwaka 2017, Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 4 wa mwaka 2017 na Muswada wa kurekebisha Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017.

Mwananchi:

Hakuna maoni: