Jumapili, 26 Novemba 2017

Mgombea Chadema alia na hujuma dhidi yake

Mgombea Udiwani wa Kata ya Saranga (Chadema), Ephraim Kinyafu amelalamikia hujuma dhidi ya mawakala wake kwa madai kwamba wameondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.

Akizungumza na waandishi leo Jumapili baada ya kupiga kura Kinyafu amesema mawakala walitakiwa kuapishwa Novemba 22 mpaka 24 lakini badala yake waliapishwa jana Jumamosi na kupewa fomu za kiapo leo leo Jumapili saa 2 asubuhi wakati wenzao wa CCM walipewa jana Jumamosi.

Amesema kuna hujuma inafanyika dhidi ya chama chake kwa kuwaondoa mawakala wenye sifa ili tu wasiwepo kwenye vituo vya kupigia kura.

“Kanuni zinaelekeza kwamba wakala anatakiwa kuwa fomu ya kiapo ya Tume ya Uchaguzi na barua ya chama. Sasa wameongeza sifa nyingine kwamba awe na kitambulisho cha mpiga kura au cha Taifa, baadhi ya mawakala wetu hawana hivyo vitambulisho, hawajaruhusiwa," amesema Kinyafu.

Mgombea huyo amesisitiza kwamba katika vituo 129 vya kupigia kura katika kata hiyo, hakuna mawakala wa Chadema, wameondolewa kwa kukosa vitambulisho.

Amesema maandalizi ya uchaguzi huo siyo mazuri na yametawaliwa na figisufigisu vinavyolenga kumkosesha ushindi.

Hakuna maoni: