Licha ya kutetea ubingwa wa Dunia, Bondia Ibrahim Class amekiri mpinzani wake alimpa tabu raundi za awali kwani alikuwa na ngumi nzito.
Class ambaye usiku wa kuamkia Novemba 26 ameandika historia nyingine kwa kutetea ubingwa wa Global Boxing Council (CBG) dhidi ya Koos Sebiya wa Afrika Kusini alisubiri hadi raundi ya tisa kuanza kuwahakikishia mashabiki wake ubingwa.
"Halikuwa pambano jepesi, mpinzani wangu alikuwa na nguvu za ajabu, nilipata wakati mgumu hasa kwenye raundi za awali, kama nisingefanya maandalizi ya nguvu basi lolote lingetokea, Koos ni bondia mwenye nguvu sana," alisema Class.
Mtanzania huyo aliyezichapa mbele ya mamia ya mashabiki kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam akiwamo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alitwaa taji hilo kwa matokeo ya pointi baada ya kumaliza raundi zote 12 kwenye uzani wa Super feather.
"Class ameonyesha uwezo mkubwa kwani mpinzani wake hakuwa bondia legelege, pambano lilikuwa zuri mno na Class katuonyesha kwamba hakubahatisha alipotwaa ubingwa huu kwa mara ya kwanza kule Ujerumani na sasa ameutetea," alisema Waziri Mwakyembe.
Katika pambano hilo, mashabiki wa Class walianza kulipuka kwa shangwe raundi ya tisa baada ya Mtanzania huyo kumtembezea kipigo 'heavy' mpinzani wake ambaye hadi anafika raundi ya 12 tayari alikuwa akivuja damu usoni licha ya kucheza raundi ya kwanza hadi ya nane kwa kujiamini hali iliyosababisha ukimya kwa muda kwa mashabiki wa Class.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni