Jumapili, 15 Oktoba 2017

Watu wawili wauwawa kwa kukatwa mapanga

Wanandoa Adam Mtembe (41) na mkewe Adalina Mtembe (39) wakazi wa kijiji cha Kasekese B Wilayani Tanganyika wameuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa kuamkia jana (Jumamosi) majira ya saa sita usiku na watu wasiojulikana.

Wakati wa tukio hilo likiendelea watoto wa marehemu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijitahidi kupambana kuwaokoa wazazi wao lakini walishindwa baada ya kushambuliwa na marungu.

Afisa mtendaji wa kijiji cha Kasekese, Ndg. Ramadhani Ibrahim amesema marehemu Adam ambaye ni mfanyabiashara kijijini hapo, siku ya tukio alifunga maduka yake mapema na kwenda kulala kama kawaida yake.

Ndg. Ramadhani amesema wanandoa hao wakiwa wamelala usiku, kulitokea watu wasiojulikana wakipiga risasi hewani karibu na nyumba yao na kuwatishia majirani wasitoke nje.

Ramadhani amesema baada ya vitisho hivyo watu hao waliingia ndani na kuanza kuwashambulia wanandoa hao kwa mapanga.

Wakati wa tukio hilo likiendelea watoto wa marehemu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijitahidi kupambana kuwaokoa wazazi wao lakini walishindwa baada ya kushambuliwa na marungu.

Mtendaji amesema majirani baada ya kusikia utulivu waliingia kwenye nyumba hiyo na kuwakuta wanandoa hao chini ya kitanda wakiwa na majeraha makubwa kwenye sehemu za uso na mikononi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kasekese B , Happiness Bona amesema walipoona watu hao wakiwa kwenye hali mbaya walifanya jitihada za kuwapeleka hospitali lakini hawakufika walifia njiani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Kamanda Damas Nyanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mpaka sasa miili ya wanandoa hao imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda Nyanda amesema kwa sasa polisi wanafanya jitihada za kuwasaka wahalifu hao kwa hali na mali.

Hakuna maoni: