Ijumaa, 22 Septemba 2017

Mahakama ya Tanzania iko huru kuliko ya Kenya - Jaji Mkuu


Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Mahakama ya Tanzania iko huru kiasi kwamba hata Kenya wanakiri kuwa ni zaidi yao.

Jaji Juma alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa majaji wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika nchini.

Hata hivyo, alisema si vyema kujilinganisha na Kenya kwa kuwa kila nchi ina historia yake, utaratibu na mfumo wake.

Alisema hatua ya Mahakama ya Juu ya Kenya kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo imetokana na mamlaka iliyopewa ambayo Mahakama ya Tanzania haina, lakini akasema Wakenya wenyewe huwa wanasema kuwa Mahakama ya Tanzania iko huru zaidi.

“Pengine hamfahamu tu nao wanatuangalia sisi vilevile, hukumu zetu ziko huru. Kwa hiyo nadhani tusijilinganishe bila kuangalia hali halisi. Sheria huwa inatungwa ili ifanye kazi katika nchi husika kulingana na mazingira. Kwa hiyo huwezi kutoa sheria ile ya Kenya ukaipandikiza Tanzania na ikafanya kazi.”

“Kwanza ningependa kusema kwamba Mahakama ya Tanzania ni huru sana, ni huru sana kimfumo, uhuru binafsi. Kutokana na mpangilio tu, Jaji Mkuu hawezi kumuamrisha hakimu, hawezi kumwingilia hakimu yeyote hata wa Mahakama ya Mwanzo na kumwelekeza atafanya nini.” alisema.

“Kwa bahati nzuri kazi zetu, kati ya mhimili ambao unafanya kazi zake kwa uwazi zaidi ni Mahakama. Kesi zetu mnaingia ukitaka kusoma ushahidi unaweza kuomba ukaenda kusoma majalada ukaangalia, hakimu akikosea unakata rufaa jalada linaweza kuitwa na kufanyiwa marejeo. Kwa hiyo shughuli zetu ni za uwazi zaidi kuliko mihimili mingine. Sisi tunajiona huru kabisa.”

Hata hivyo, alisema changamoto inayowakabili ni mtazamo wa watu wa nje akisema vinaweza kutokea vitendo nje ya Mahakama na watu kutegemea Jaji Mkuu atoe tamko au aingilie.

Alisema wakati mwingine wamekuwa wakiwakatalia wanasiasa ambao wamekuwa wakiwaandikia wakiwaomba kuingilia jambo fulani, wakiwaeleza kuwa Mahakama ina utaratibu wake.

“Mahakama haifanyi kazi barabarani au kwenye mitandao. Kuna njia za kuja mahakamani. Kuna vyama vya siasa huwa vinatuandikia barua Jaji Mkuu ingilia hivi kuna hivi, lakini mimi huwa nawajibu kuwa kuna utaratibu wa kuomba nafuu za Mahakama.

“Pale ndio utapata nguvu ya Mahakama. Lakini mimi Jaji Mkuu au Jaji Kiongozi akichukua simu na kumpigia hakimu kuwa fanya hiki, hakimu atakataa na atakuwa na haki ya kukataa. Kwa hiyo uhuru wa mahakama kwa kweli upo.”

Kuhusu mkutano huo wa majaji na mahakimu wa Jumuiya ya Madola, alisema utakuwa kuanzia Septemba 24 hadi 28 na utafunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na utafungwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Alisema kaulimbiu ya mkutano huo utakaoshirikisha majaji wakuu 13, ni ‘Mahakama Madhubuti, Inayowajibika na Jumuishi’.

Alisema pia kutakuwa na washiriki sita mashuhuri ambao ni marais waandamizi wa Mahakama za Juu na za Rufaa ndani na nje ya Afrika na mahakimu na majaji kutoka nchi za Jumuiya ya Madola na kwamba washiriki 354 wameshajisajili.

Rais wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Jaji Ignas Kitusi alisema mkutano huo utalinufaisha Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwamo utalii kwani wameshirikisha idara na taasisi nyingine ikiwamo Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hakuna maoni: